Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Ludovick Nduhiye ameutaka uongozi wa chuo cha Taifa cha Usafiraji (NIT) kuhakikisha wanatunza na kuendeleza vifaa kwa ajili ya mafunzo ya Urubani, Wahudumu wa ndani ya Ndege na Wahandisi Matengenezo ya ndege.
Nduhiye amesema hayo tarehe 9.5.2025 baada ya kutembelea na kukagua vifaa mbalimbali vilivyonunuliwa na Serikali katika kufundishia mafunzo ya Marubani na Wahudumu wa ndani ya Ndege.
“Serikali imewekeza fedha nyingi katika kununua vifaa hivyo vya kufundishia marubani hivyo uongozi wa Chuo unatakiwa kuhakikisha vifaa hivi vinatunzwa ili vidumu kwa muda mrefu” Alisema Nduhiye.
Pamoja na kukagua na kutembelea vifaa hivyo pia alikagua ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa kike na wakiume majengo ya utawala ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 98 na unatarajiwa kukamilika katika mwaka huu.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Dkt. Prosper Mgaya amesema kuwa vifaa vyote vya kufundisha urubani katika chuo vimekamilika na mafunzo hayo yanatarajia kuanza Mwezi sita mwaka huu. Aidha ameushukuru Uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yote kwakuwa wamewezesha ununuzi wa vifaa hivyo.
“ Vifaa vya kufundishia Urubani vimekamilika na tumeshapata idhini kutoka mamlaka ya Usimamizi wa Anga (TCAA) kuanza kufundisha hivyo tunatarajia kuanza kutoa mafunzo haya mwezi wa sita na tuanza na wanafunzi kumi na mbili” Alisema Mgaya
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo hicho Prof. Ulingeta Mbamba amesema Baraza la chuo litaendelea kusimamia Ubora wa Elimu unaotolewa na chuo hicho kwa masomo yaote ili chuo hicho kiendelee kutoa wataalam wanaoweza kushindana katika soko la ajira za ndani na nje ya nchi.
Mkufunzi wa Mafunzo ya wahudumu wa ndani ya Ndege amesema kuwa vifaa vyote vya wahudumu wa ndege vipo tayari kwa ajili ya kufundishia hivyo anawakaribisha vijana kwenda katika chuo hicho kupata mafunzo hayo katika Sekta ya Anga.