Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) leo, Novemba 11, 2026, kimekabidhi rasmi Ofisi ya Serikali ya Mtaa Mabibo iliyojengwa na Chuo kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za kijamii na kiutawala kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka chuo pamoja na wanafunzi wake.
Ofisi hiyo imekabidhiwa rasmi kwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi na makabidhiano. Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Msando amepongeza uongozi wa NIT kwa kuonesha mshikamano na ushirikiano na Serikali za Mitaa katika kuchangia maendeleo ya jamii.
“Niipongeze Chuo cha Taifa cha Usafirishaji kwa hatua hii ya kujenga na kukabidhi ofisi hii ya Serikali ya Mtaa. Huu ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya Taasisi za umma na Serikali za Mitaa katika kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema Mhe. Msando.
Ameongeza kuwa uwepo wa ofisi hiyo utarahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiutawala, sambamba na kuboresha usimamizi wa masuala ya wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka chuo.
Aidha, Mkuu wa Chuo, Dkt. Prosper Mgaya, amesema ujenzi wa ofisi hiyo ni sehemu ya jitihada za chuo katika kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Mtaa kwa kutambua umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja katika kutatua changamoto za kijamii na kuboresha utoaji wa huduma.