Fri, 01 May 2026 | 09:47 AM
Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Mha.Dkt. Prosper Mgaya amekabidhi zawadi mbalimbali kwa wafanyakazi bora na hodari wa Chuo kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Watumishi hao wamekabidhiwa zawadi zao ikiwemo fedha taslimu na vyeti tarehe 30 Aprili 2026.
Akizungumza na watumishi wa Chuo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi zawadi kwa wafanyakazi bora na hodari iliyofanyika katika ukumbi wa MPH uliyopo katika kampasi ya Chuo Mabibo Jijini Dar es salaam Dkt. Mgaya amewapongeza wafanyakazi kazi hao kwa kuibuka washindi katika zoezi la kuchagua wafanyakazi bora na hodari wa Chuo lililofanyika hivi karibuni baada ya kuidhinishwa kwa Mwongozo wa Jinsi ya Kumpata Mfanyakazi Bora na Mfanyakazi Hodari wa Chuo.
"Kwa niaba ya Uongozi wa Chuo nawapongeza watumishi wote waliochaguliwa kuwa wafanyakazi bora na hodari katika mwaka huu wa fedha,huu ni mwanzo mzuri natumaini mtakiwakilisha vizuri Chuo katika zoezi la utoaji wa tuzo wakati wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani kitaifa"
Aidha, Dkt.Mgaya amewahakikishia watumishi wa Chuo kuwa zoezi la kutoa motisha mbalimbali kwa wafanyakazi bora na hodari wa Chuo kuwa endelevu na kuboreshwa zaidi.
"Huu ni mwanzo tuu, tutaendelea na utaratibu huu mwakani na kufanya maboresho mbalimbali"
Zoezi la kuchagua wafanyakazi bora na hodari wa Chuo limehitimishwa leo kwa washindi kutangazwa na kukabidhiwa zawadi zao ambapo Mha.Castor Njako ameibuka mfanyakazi hodari wa Chuo, Bi.Rehema Mzee (mfanyakazi bora kada ya wanataaluma),Bw.Meshack Kimaro(mfanyakazi bora kada ya waendeshaji),na wafanyakazi bora katika kundi la ushindani akiwemo Bw.Honest Mrosso, aBw.Robert Kilamato,Bw.Michael Soka,Bw.Juma Msemwa, na CPA.Innocent Mshanga.